Elimu ya ufugaji kuku wa kienyeji kitaalamu zaidi

Sifa za Kuku wa Asili:
a. Ni vigumu sana kukumbwa na magonjwa, Ingawa kuwapatia kinga ni muhimu ili kuwaepusha na baadhi ya magonjwa kama mdondo, ndui nk. ili kuweza kuwaendeleza.
b. Wana uwezo wa kujitafutia chakula ardhini, japo haimzuii mfugaji kuandaa chakula
c. Wana uwezo wa kuatamia mayai, kutotoa, kulea vifaranga na ustahimilivu wa mazingira magumu (ukame, baridi nk).
d. Mazao yake kama Nyama na mayai yake vina ladha nzuri kuliko kuku wa kisasa.
e. Kwa kiasi fulani wana uwezo wa kujilinda na maadui kama vile mwewe. Pamoja na sifa hizi ni muhimu kuku hao wakapewa matunzo mazuri, wawekwe kwenye mabanda mazuri na imara, pia wapewe maji na chakula cha kutosha.

 Faida za Ufugaji wa Kuku wa Asili:
a. Chakula – nyama ya kuku na mayai hutumika kama chakula muhimu cha wanadamu, chenye protini.
b. Chanzo cha kipato – mkulima hupata fedha akiuza kuku au mayai.
c. Chanzo cha ajira – ufugaji wa kuku hutoa ajira kwa jamii.
d. Kuku hutumika kwenye shughuli za ndoa kama vile kutoa mahari na pia ni kitoweo muhimu katika sherehe hizo.
e. Gharama nafuu za kuanzisha na kuendesha mradi huu.
f. Ni kitoweo rahisi na chepesi kwa wageni kuliko wanyama wakubwa kama ng’ombe au mbuzi.
g. Ni kitoweo kisichohitaji hifadhi, hutumika mlo mmoja au miwili na kumalizika.
h. Kuku na mayai hutumika kwa tiba za asili.
i. Jogoo hutumika kama saa anapowika nyakati za alfajiri na majira mengine ya siku.
 j. Hutuhabarisha iwapo kiumbe kigeni au cha hatari kwa mlio maalum wa kuashiria hatari.
k. Mbolea – kinyesi cha kuku kinaweza kutumika katika kurutubisha mashamba ya mazao na mabwawa ya samaki.
l. Kuendeleza kizazi cha kuku wa asili hapa nchini.
m. Soko lipo la uhakika, ukilinganisha na kuku wa kisasa kwani nyama na mayai yake hupendwa zaidi na walaji.
n. Manyoya ya kuku hutumika kama mapambo, pia huweza kutumiaka kutengenezea mito ya kulalia na kukalia.
o. Shughuli za utafiti – kuku wanatumika katika tafiti nyingi za baiolojia, kama kutambua mambo ya lishe.
p. Shughuli za viwandani: • Mayai yenye mbegu ya jogoo hutumika katika kutengeneza dawa za chanjo. • Magamba ya mayai yanaweza kutumika katika utengenezaji wa vyakula vya wanyama. • Kiini cha njano cha mayai kinaweza kutumika kutengeneza mafuta ya kuoshea nywele (shampoo).

 Mapungufu ya Kuku wa Asili:
a. Hutaga mayai madogo wastani wa gramu 47 ambapo kuku wa kisasa wastani wa gramu 55, aidha hutaga mayai machache wastani wa mayai 60 kwa mwaka ambapo kuku wa kisasa huweza kutaga hadi mayai 300 kwa mwaka.
b. Ukuaji taratibu – kuku wa asili hukua taratibu kutokana na lishe duni. Kutokana na hali hiyo kuku huchukua muda mrefu (miezi sita) kufikia uzito wa kuchinjwa (kilo 1 - 1.5). Hali hii pia hufanya faida ya ufugaji wa kuku wa asili kuchukua muda mrefu kupatikana.
c. Nyama yake ni ngumu (huchukua muda mrefu kuiva) ikilinganishwa na kuku wa kisasa.

 Changamoto katika ufugaji kuku wa asili:
a. Mabanda: Ukosefu wa mabanda bora.
 b. Wezi, wanyama na ndege hushambulia kuku.
c. Magonjwa: kama mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku.
d. Tabia na miiko ya baadhi ya jamii. Baadhi ya jamii za makabila hapa nchini huona ufugaji wa kuku kama ni kitu duni.
e. Upatikanaji haba wa chanjo za magonjwa kama vile, mdondo, ndui, homa ya matumbo.

No comments:

Post a Comment