Kilimo bora cha mpunga kwa njia za kisasa

ELIMU MHIMU KUHUSU ZAO LA MPUNGA Mpunga ni zao la pili la chakula kwa umuhimu linalolimwa sehemu nyingi nchini Tanzania likiongozwa na zao la Mahindi . Umuhimu wa zao hili umeongezeka kuanzia muongo uliopita kutokana na jamii za mijini na vijijini kupendelea zaidi kula wali na kupunguza ulaji wa vyakula vingine na kulifanya zao hili kuwa la chakula na biashara. Mazingira yanayofaa kwa kulima mpunga Mvua ni chanzo kikuu cha maji kwenye kilimo cha mpunga. Viwango vya mahitaji ya maji katika kukua kwa mpunga hutofautiana miongoni mwa aina za mpunga. Ni kwa jinsi hii mpunga hupandwa katika mazingira mbalimbali kutegemea na mahitaji yake ya maji. Zipo aina tatu kuu za mazingira yanayolimwa mpunga kulingana na upatikanaji wa maji na hali ya mwinuko wa nchi. Mazingira haya ni kilimo cha mpunga wa mabondeni kinachotegemea mvua (72%), kilimo cha mpunga wa kwenye miinuko (20%) na kilimo cha mpunga cha umwagiliaji (8%). Kiasi cha mpunga kinachozalishwa nchini kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka tani 41,000 mwaka 1970 hadi tani 811,500 mwaka 1998. Ongezeko hili limetokana na kuongezeka kwa eneo linalolimwa mpunga na kwa kiasi kutokana na kuongezeka kwa miradi midogo ya umwagiliaji pamoja na matumizi ya teknolojia bora za kilimo. Maeneo yanayolima mpunga Maeneo yanayolima mpunga kwa wingi Tanzania ni; Morogoro maeneo ya bonde la kilombero/Ifakara, Dakawa, Malolo; Mbeya: Kyela, Mbarali; Shinyanga: Kahama; Mwanza, Bonde la Ruvu mkoani Pwani. Na maeneo mengine mengi. Sehemu ya shamba la mpunga uliostawi vizuri pH ya udongo (Soil pH) inayofaa kwa Mpunga pH ni kipimo kinachoonyesha kiwango cha tindikali au nyongo katika udongo. Udongo waweza kuwa tindikali (ph ndogo kuliko 7), nyongo (ph kubwa kuliko 7), au katikati (neutral) – ph ya 7. Tindikali au nyongo ya udongo hupimwa kwa kutumia pH mita. Mazao mengi hustawi zaidi katika udongo wenye hali ya tindikali ya wastani (kipimo cha pH 5.5 hadi 7.0). Mpunga hustawi kwenye udongo wa mfinyanzi wenye tindikali ya wastani na virutubisho vya kutosha. Maandalizi ya shamba la Mpunga Ni vyema mashamba yaandaliwe mapema kabla ya msimu wa kupanda haujaanza ili kumpa mkulima fursa ya kupanda kwa wakati unaotakiwa. Kuna njia mbalimbali zinazotumika kuandaa mashamba. Kati ya njia hizi ni pamoja na kufyeka, kung’oa visiki na kulima. Shamba linaweza kulimwa kwa kutumia: Jembe la mkono – wengi wanatumia Jembe la kukokotwa na wanyama kama ng’ombe Power tillers Matrekta Baaada ya kulima, shamba linawekwa maji ili liloane vizuri na kisha udongo unachanganywa vizuri na maji ili kutengeneza tope. Hii inafanyika kwa kuvuruga au kuchavanga (puddling). Hii inarahisisha kupandikiza miche na kuhifadhi maji. Aina za Mbegu za Mpunga Matumizi ya mbegu bora ni muhimu katika upatikanaji wa mavuno mengi na bora. Kuna makundi mawili makuu ya mbegu za mpunga ambayo ni: 1. Mbegu za asili za mpunga Ni zile ambazo zimetumika miaka mingi katika historia ya kilimo. Kuna aina nyingi za mipunga ya asili inayolimwa sehemu mbalimbali hapa nchini kama Supa, Kahogo, Kula na Bwana, Shingo ya mwali, n.k. Wakulima wanazipenda mbegu hizi kutokana na kuwa na sifa kama vile ladha nzuri, uvumilivu wa matatizo mbalimbali ya kimazingira na kwa sababu ya uwezo wa mbegu hizi kustahimili katika hali mbaya ya hewa na hazihitaji uangalizi wa hali ya juu. Sifa hizi ni matokeo ya mbegu hizi kumudu mazingira na uchaguzi wa mbegu uliofanywa na wakulima kwa miaka mingi. Hata hivyo, nyingi ya mbegu hizi zina uwezo mdogo wa kuzaa, zinachelewa kukomaa, ni ndefu na rahisi kuanguka. 2. Mbegu bora za mpunga Hizi ni zile zilizoboreshwa kutokana na mbegu za asili. Mfano wa mbegu za mpunga zilizoboreshwa ni kama vile Katrin, IR54, na IR64. Zinazaa sana hasa kwa kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo, hazikidhi ladha ya walaji na ukobolekaji wake si mzuri na baadhi hazistahimili kwenye mazingira mengi ya kawaida. Hii imezifanya mbegu hizi kukubalika na wakulima kwa kiwango kidogo sana. Mbegu bora nyingine zilizozalishwa kutoka utafiti na kuonekana kupendwa kwa ajili ya mavuno mengi na ladha nzuri ni kama TXD88 na TXD85. Mbegu ya SARO 5 (TXD306) Hivi karibuni imetolewa mbegu nyingine inayoitwa TXD306 au kwa jina maarufu SARO 5. Mbegu hii ya mpunga inapendwa sana na wakulima, wafanyabiashara na walaji. Hii ni kutokana na sifa yake ya kutoa mavuno mavuno mengi, punje ndefu kiasi na nzito, ladha nzuri na yenye kunukia pindi ipikwapo na kuliwa. Mbolea za kupandia mpunga Mbolea zinazofaa kupandia mpunga ni zile zenye kirutubisho cha P (phosphate), ambazo ni kama MAP, DAP au Minjingu Mazao. Viwango vya mbolea za kupandia Kiwango cha mbolea za kupandia kinachopendekezwa ni kilo 20 phosphate (P) kwa hekta moja ambayo ni sawa sawa na mifuko mitatu ya DAP kwa hekta (= mfuko mmoja kwa ekari). Hii ni sawa na mifuko miwili kwa hekta ya Minjingu Phosphate (= mfuko mmoja na nusu kwa ekari) au mifuko minne na nusu kwa hekta ya Minjingu Mazao (= mifuko miwili kwa ekari). Wakati wa kuweka mbolea za kupandia Mbolea ya kupandia mpunga iwekwe kabla ya kupanda mbegu za mpunga au kupandikiza miche ya mpunga. Kabla ya kuweka mbolea hakakisha kuwa majaruba yanatengenezwa ili kuhakikisha maji hayaingii na kutoka kiholela. Mbolea ya kupandia mpunga huwekwa kwa kusia katika jaruba kabla ya kuchavanga. Kuchavanga husaidia kuchanganya udongo na mbolea na pia kutengeneza eneo zuri la kupandikiza miche. Baadaye miche hupandikizwa. Upandaji wa Mpunga Njia za upandaji wa mpunga Kitaalam, kuna njia mbili kuu zinazotumika kupanda mpunga shambani. Njia hizo ni ile ya kupanda mbegu moja kwa moja na ile ya kupandikiza miche. 1. Kupanda mbegu moja kwa moja Njia hii hutumika kwa kupanda mbegu za mpunga moja kwa moja kwenye shamba lililotayarishwa vizuri. Njia ya kawaida (ya kienyeji) wanayoitumia wakulima ni ile ya kumwaga kwa kuzitawanya mbegu (yaani broadcasting) na kuzifukia mbegu. Njia ya kitaalam ni ile ya kupanda mbegu kwenye mashimo yaliyo kwenye mistari na kwa kuzingatia nafasi maalum. Lakini pia mbegu zinaweza kupandwa kwenye mashimo yaliyoandaliwa bila kufuata mstari wala kuzingatia nafasi iliyopendekezwa (dibbling). Vile vile mbegu za mpunga huweza kupandwa kwa kunyunyizwa kwenye vifereji vyenye vina vifupi na kufukiwa pasipo kuwa na nafasi maalum kati ya punje na punje (seed drilling). 2. Kupandikiza miche ya mpunga Njia hii hutumika kwa kupanda mbegu kwanza kwenye kitalu kabla ya kuzihamishia shambani. Mara nyingi mbegu za mpunga hutumia wiki mbili hadi tatu baada ya kuota kwenye kitalu ili kufikia umri wa kupandikizwa shambani. Katika shamba, miche ya mpunga huweza kupandikizwa kwa kufuata mistari na kwa nafasi maalum au kwa kufuata mistari tu bila nafasi maalum au kupandikizwa kiholela bila kuzingatia nafasi maalum za kupandia. Inashauriwa kupandikiza miche katika kina cha sentimeta 2 hadi 3. Ukipanda kina kirefu machipukizi huchelewa kujitokeza. Baada ya kupandikiza miche, machipukizi hujitokeza baada ya siku 5 hadi 10. Kupandikiza miche ya Mpunga Nafasi ya kupanda mpunga Kama unatumia mbegu za asili, panda mpunga kwa kutumia nafasi ya sm 20 kwa sm 20 au sm 25 kwa sm 25 au sm 30 kwa sm 30. Na ikiwa unatumia mbegu bora inashauriwa kutumia nafasi ya sm 15 kwa sm 15 au sm 20 kwa sm 20. Kwenye mpangilio wa mistari miwili miwili (double rows), nafasi kati ya mistari miwili ni sm 10, na nafasi kati ya mimea katika kila mstari ni sm 20, na nafasi kati ya mistari miwili na mistari miwili mingine (double rows) ni sm 40. Kupanda kwa nafasi ni kati ya njia bora za kilimo inayomwezesha mkulima kupata mazao bora. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kupanda kwa mistari na kufuata nafasi zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo. Wakati kupanda Mpunga Muda wa kupanda unatofautiana kutoka eneo moja hadi jingine kulingana na majira ya mvua. Kwa mfano katika wilaya ya Morogoro tarehe za kupanda ni kuanzia Desemba hadi Januari kwa mpunga wa muda mrefu. Kwa mpunga wa muda wa kati na muda mfupi, tarehe za kupanda ni Februari hadi Machi. Kupalilia Mpunga Ni muhimu shamba lipaliliwe ili kuondoa magugu. Magugu ni mimea hivyo hushindana na mimea iliyopandwa na mkulima kwa kunyonya virutubisho ardhini. Magugu yanaweza pia kuhifadhi wadudu na magonjwa yanayoweza kushambulia mimea iliyopandwa na hivyo kupunguza mavuno. Katika kilimo cha mpunga, ni muhimu shamba lipaliliwe siku 14 hadi 21 baada ya mimea kuota kufuatana na hali ya shamba wakati wa kupanda. Ni vizuri katika kilimo cha mpunga, shamba lipaliliwe mara mbili, kutegemeana na hali ya magugu katika shamba. Unaweza kupalilia kwa kung’olea kwa mkono, kwa mashine au kwa kutumua viua magugu (herbicides) kama vile 2, 4-D (Two Four D). Utafiti unaonyesha kwamba, shamba la mpunga ambalo halijapaliliwa linaweza kupunguza mavuno kwa asilimia 60 hadi 100 ya mavuno yanayotarajiwa. Hata kama mkulima atatumia mbegu bora, aina na kiasi cha mbolea zinazoshauriwa, kupanda kwa mstari pamoja na mbinu nyingine bora zinazoshauriwa, bila kupalilia hali hii itaathiri mavuno yake. Mbolea za kukuzia mpunga Ni mbolea zinazotumika baada ya mimea kuota kwa lengo la kuikuza mimea ili itoe mavuno bora. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha naitrojeni. Kiwango kinachopendekezwa ni kilo 60 naitrogeni kwa hektari, ambacho ni sawasawa na kiasi cha mifuko miwili ya UREA au Minne na Nusu Ya CAN au Mitatu ya SA. Mbolea inayotumika mara kwa mara ni Urea. Hata hivyo mbolea zingine kama SA inaweza kutumika kama kuna mahitaji ya salfa. CAN inaweza kutumika kama kuna mahitaji maalum ya nitrate na ammonium. Kwenye mpunga, mbolea ya kukuzia inawekwa wiki mbili baada ya kupandikiza miche na irudie tena baada ya wiki nne. Kuweka mbolea: Mbolea ya kukuzia hutiwa kwa kusia wiki mbili baada ya kupandikiza, na kurudia mwezi mmoja baadaye. Ni vyema kuweka mbolea za kukuzia mara mbili ya kiasi kinachopendekezwa. Shamba la mpunga uliopandwa kwa mistari Kudhibiti Magonjwa na Wadudu Wanaoshambulia Mpunga Magonjwa Yanayoshambulia Mpunga Magonjwa ya mpunga yamegawanyika katika makundi matatu kulingana na vimelea visababishi ambavyo ni fungasi, virusi na bakteria. i) Rice blast (Ukungu) Unaosababishwa na Pyricularia oryzae. Dawa/Kudhibiti: Mbegu bora inayostahimili ugonjwa, kupanda mapema, kung’oa mimea iliyoathirika ama kunyunyiza dawa za kuua ‘vectors’ kama vile inzi weupe (white flies). ii) Brown leaf spot Unaosababishwa na Helminthosporium spp. Dawa/Kudhibiti: Panda mbegu kwa udongo unaofaa, weka mbolea ya kuzuia au tibu mbegu na dawa. iii) Sheath rot Unaosababishwa na Acrocylindrium oryzae. Dawa/Kudhibiti: Kwa sasa hakuna njia ya kuzuia iv) Rice Yellow Mottle Virus (RYMV) – Kimnyanga Hivi karibuni ugonjwa wa kimyanga umetajwa kama ugonjwa hatari sana kwa mpunga hapa Tanzania. Dawa/Kudhibiti:  Panda mbegu zilizoboreshwa, zinazostahimili magonjwa au ng’oa mimea iliyoathirika. Magonjwa yasababishwayo na bakteria nayo wametajwa kuwa na madhara makubwa kwa uzalishaji wa mpunga hapa nchini. Bakteria hawa wanajumuisha Acidovorax avenae subsp. Avenae asababishae ugonjwa wa bacterial stripe, Pantoea aglomerans, asababishae ugonjwa wa palea browning na Xanthomonas oryzae p.v. oryzae. Wadudu wanaoshambulia mpunga Kuna aina nyingi sana za wadudu wanaoathiri mpunga katika hatua mbalimbali za ukuaji wa mpunga. Wanapokithiri na wasipodhibitiwa hupunguza kiasi cha mavuno shambani. i) White flies (Funza weupe) Dawa/Kudhibiti: Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Regent 3G), Fenthion (k.m. Lebaycid) ii) Rice stalk borer waharibifu Kudhibiti: Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Re­gent 3G), Fenthion (k.m. Lebaycid) Ili mkulima aweze kupata mazao mengi na bora inashauriwa kutumia dawa za kuzuia magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea na njia zinginezo. Kuvuna, Kukausha, Kusafisha na Kuhifadhi Mpunga Kuvuna: Mpunga uko tayari kuvuna wakati asilimia themanini (80%) ya rangi ya mpunga kwenye masuke imebadilika na kuwa dhahabu. Mpunga unavunwa kwa kukata bua pamoja na suke lake. Uvunaji wa mpunga Kukausha: Rundika pahali pakavu k.m. kwenye tuta la jaruba halafu pigapiga (thresh) ili kutenganisha masuke na mpunga. Kama mpunga hayajakauka vizuri hukaushwa zaidi juani kwa siku 3-4 ili kupunguza unyevunyevu kufikia kiwango kinachofaa kwa kuhifadhi (14%). Ni muhimu mpunga ukauke vizuri ili usioze ukiwekwa ghalani. Kusafisha:  Mpunga uliyokauka vizuri hupepetwa na vilevile mapepe huondolewa. Kuhifadhi: Mpunga safi huwekwa kwenye gunia na magunia kupangwa vizuri ghalani juu ya mbao yasiguse sakafu. Prepared by Jafaido Group Ltd Adam Shayunga Managing Director Phone: 0765364627

No comments:

Post a Comment